Sunday, July 25, 2010

Mbunge mtarajiwa kupitia Chadema aliyenaswa na mguu wa mtu aliza makanisa

Baadhi ya waumini wa makanisa mbalimbali mkoani hapa, wako katika kilio kufuatia kitendo cha mgombea Ubunge wa Chadema aliyerudisha fomu, George Mtasha (50) kudakwa na jeshi la Polisi wilayani Chunya akiwa na mguu wa kushoto wa binadamu, Risasi Jumamosi linashuka kikamilifu.

Wakiongea na Mwandishi Wetu, baadhi ya waumini hao walisema kuwa, wanaamini kitendo hicho ni ishara ya mwanzo wa vitendo viovu ambavyo vimekuwa vikiukumba mkoa wa Mbeya miaka ya karibuni.

Josephat Mwaibabile ambaye ni Mzee wa Kanisa la Kiroho la Jerusalem Temple, alisema kuwa mkoa wa Mbeya una skendo ya watu kuchunwa ngozi, waumini wakalia kwa Mungu kwa maombi na kufunga mpaka mambo yakakaa sawa, “Sasa hili la mtu kukutwa na mguu wa binadamu mwenzake, nalo limetuliza, Mungu apishie mbali jamani,” alisema mzee huyo.

George Mwangata, muumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (chini ya Askofu Mkuu, Alex Malasusa) Soko Matola, jijini humu, alisema kitendo cha mtuhumiwa kukutwa na kiungo hicho ni pigo kwa makanisa, kwani Mbeya ndiyo mkoa unaoongoza kwa kuwa na makanisa mengi nchini Tanzania.

Mama Nitike, muumini wa Roman Catholic (chini ya Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo), Mwanjelwa, Manispaa ya Mbeya, alisema alishtuka kusikia habari hizo na hajaamini kama kweli kiungo hicho kilikuwa ni cha binadamu.
“Kwa kweli sijaamini, he! Kweli binadamu unatembea na kiungo cha binadamu mwenzako, mh!” Alishangaa sana mama Nitike.

Aidha, Risasi Jumamosi lilipata bahati ya kuongea na Paulina Mwakifwamba, muumini wa Kanisa la Anglican (chini ya Askofu Costantine Mokiwa pichani), Rungwe ambapo alisema kuna haja ya umoja wa makanisa mkoani humo kukaa haraka na kufanya maombi ya kufunga siku tatu ili kumwomba Mungu aondoe roho inayotaka kuinuka, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.

Naye muumini wa kanisa la Full Gospel&Bible Fellowship (FGBF) ambalo lipo chini ya Askofu Mkuu, Zacharia Kakobe, aliyejitambulisha kwa jina moja la Frank, tawi la Mbeya alisema maombi ya kufunga yanatakiwa kwa ajili ya mwelekeo mzima wa uchaguzi mkoani humo, mbali na suala la mgombea huyo kukutwa na mguu wa binadamu.

George Mtasha ni mgombea Ubunge jimbo jipya la Makongorosi, wilayani Chunya na mwenzake, Paul Mnyambwa, walikutwa na kiungo hicho saa 12.50 alfajiri ya Jumatano, Julai 21, 2010 na kushikiliwa na jeshi la polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Advocate Nyombi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema, uchunguzi mkali unaendelea.

No comments:

Post a Comment