Friday, November 13, 2009


Mimi sivuti na lengo langu hapa siyo kuwatetea wavuta sigara. Wanasayansi wameshathibitisha kwamba uvutaji wa sigara ni tabia ya hatari inayoua mamilioni ya watu kila mwaka kutokana na saratani ya mapafu na magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa upumuaji. Kutokana na sababu hii uvutaji wa sigara umepigwa marufuku karibu katika kila kona ya dunia. Sehemu zingine zimefikia hatua ya kutunga sheria zinazowabana wavuta sigara kutovuta hata wakiwa majumbani mwao. Mwezi uliopita chuo kikuu cha Florida kilipitisha sheria ambayo inapiga marufuku uvutaji wa sigara katika maeneo yote ya chuo – ndani na nje. Sijui wavuta sigara watafanyeje!

Swali langu ni hili: mbona tumekomalia sana sigara utafikiri kwamba uvutaji ndiyo tabia pekee-angamizi? Mbona tabia zingine za hatari kama unywaji wa bia (ambao pia, mbali na matatizo mengine, umeshathibitishwa kuwa kisababishi kimojawapo kikuu cha aina mbalimbali za saratani na hasa zile za matumbo) hatuzikomalii kama uvutaji sigara? Vipi kuhusu ulaji wa nyama hasa zile “nyekundu” ambao nao pia umeshathibitishwa kwamba ni hatari kwa afya? Wavuta sigara wanaonewa?


Mimi ni mmoja kati ya watu wasiopenda tabia za kinafiki za kujifanya kuchukia tabia moja angamizi na kukumbatia zingine za aina hiyo hiyo. Ndiyo maana huwa sielewi mtu anaponiambia eti ameamua kuacha kula nyama ili kulinda afya yake na wakati huo huo anazitandika bia sawasawa, kuvuta sigara na hata kuwa “kiwembe”.


Ni mawazo yangu tu. Pengine mwanafalsafa Kitururu angeweza kusema ninachojaribu kukisema hapa kwa ufasaha zaidi!


Wasikilize watafiti hapa wakijadili athari za ulaji wa nyama, uvutaji wa sigara na unene wa futufutu (obesity) kwa afya.

No comments:

Post a Comment